Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Dionis Myinga, amefanya kikao maalum na watumishi wote wa Halmashauri hiyo katika ukumbi wa mikutano, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, nidhamu ya kazi na ufuatiliaji wa miongozo ya Serikali katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Kikao hicho, kilichohudhuriwa na watumishi kutoka idara na vitengo vyote, kililenga kuwakumbusha kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuonesha weledi unaoendana na nafasi zao.
Myinga alibainisha kuwa kila mfanyakazi ni kiungo muhimu katika safari ya maendeleo ya wilaya hiyo, na kila mwananchi anayehudumiwa Halmashauri ya Hai anapaswa kupata huduma bora bila urasimu.
Pia, aliwakumbusha watumishi wote kufuata taratibu, sheria, na miongozo ya utumishi wa umma ili kulinda taswira ya Serikali kwa wananchi.
Aidha, aliwataka kila mtumishi kuonesha kwa vitendo uwajibikaji kazini kufuatia nyongeza ya mishahara iliyotolewa na Serikali kwa watumishi wote nchini.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Halmashauri, Bakarani Urio, aliwahimiza watumishi wote kutumia mfumo wa PEPMIS (Public Employees’ Performance Management Information System).
Alieleza kuwa mfumo huo unarahisisha ufuatiliaji na tathmini ya utendaji kazi wa watumishi kwa wakati, unaimarisha uwajibikaji, na hutoa taarifa sahihi kwa ajili ya maamuzi ya kiutawala.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa wito wa mshikamano na mshirikiano miongoni mwa watumishi, ambapo ilisisitizwa kuwa maendeleo ya Wilaya ya Hai yanategemea jitihada za pamoja za kila idara na kada.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai