Serikali Yatumia Milioni 300 Kuimarisha Upatikanaji Maji Wilaya ya Hai
Imetumwa: July 10th, 2021
Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro ikiwemo mradi wa Maji utakao wanufaisha zaidi ya Kata sita Wilayani humo.
Mradi huo umegarimu zaidi ya Milioni 300 utakamilika ndani ya mwezi mmoja toka sasa na utatoa huduma ya Maji katika kata za Bomang'ombe,Bondeni, Muungano,Kia, pamoja na Kata nyingine za jirani .
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Hai Emanuel Mwampashi amesema kuwa atahakikisha Ujenzi huo unakamilika ndani ya muda ulio pangwa ili Wananchi waweze kunufaika nao huku akisema kuwa fedha zilizo tolewa na Serikali zitatumika kama ilivyo kusudiwa.
Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali anayo iongoza kwa jimsi anavyo litizama jimbo kwa jicho la upekee katika kutatua changamoto za jimbo hilo.
"Nimshukuru sana mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anatuangalia wanahai kwa jicho la upekee, sisi tunasema hatutomuangusha". Alisema Saashisha Mafuwe.
Hata hivyo Mbunge Mafuwe amesema kumekuwepo na Malalamiko kutoka kwa Wananchi kuwa zipo mita ambazo hazisomwi na wamekuwa wakipelekewa Bili za maji jambo ambalo ni usumbufu kwa wananchi.
Mbunge Mafuwe amesema atahakikisha anaendelea kutatua changamoto zilizopo katika Jimbo hilo ili Wananchi waweze kukiamnini chama cha Mapinduzi CCM.
Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Hai Kumotola Kumotola na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Salleh Kombo wamesema kwa sasa jimbo la Hai kipaumbele chake ni kutekeleza yale yaliyoainishwa katika ilani ya chama cha mapinduzi ikiwemo kuwaletea wananchi maendeleo.
Jimbo la Hai hasa ukanda wa tambarare limekuwa likikumbwa na changamoto za maji japo changamoto hizo kwa sasa zimeanza kupotea baada ya serikali kuzitatua kwa kiasi kikubwa.