Serikali imetumia shilingi Bilioni 24.8 kwajili ya kuboresha miundo mbinu ya shule za Msingi na Sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Hai, hatua inayotajwa kuchochea ongezeko la ufaulu na kupunguza changamoto za mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Kati ya fedha hizo shilingi 14,224,066,078.75 ni kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya shule na shilingi na shilingi 10,573,828,854.41 ni kwa ajili ya elimu bila malipo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Dionis Myinga ameeleza kuwa miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni ujenzi wa shule mpya 7 ambapo shule tano ni za Sekondari na shule 2 ni za awali na msingi, utanuzi na ukarabati wa shule kongwe na chakavu 5, ujenzi wa mabweni 18, mabwalo 2, matundu ya vyoo 311, nyumba za waalimu 15 madarasa 221 na maabara 17.
Myinga amesema ujenzi wa miradi hiyo imesababisha ongezeko la idadi ya wanafunzi kutoka 15,698 mwaka 2021 hadi wanafunzi 17,413 kwa shule za msingi ambalo ni sawa na asilimia 10.9 ya wanafunzi 15,698 waliosajiliwa mwaka 2021.
Ufaulu umeendelea kuongezeka katika mitihani ya kitaifa kutoka asilimia 91 mwaka 2021 hadi asilimia 98.3 mwaka 2024 kwa shule za sekondari amesema Myinga.
Wakizungumzia hatua hiyo wananchi wa Hai wameishukuru serikali na kusema kwamba imewapunguzia wanafunzi umbali wa kutembea ambapo awali baadhi ya wanafunzi walikuwa wakitembea zaidi ya umbali wa hadi km 15 kwa siku.
“Watoto wetu walikuwa wanatembea umbali mrefu, wanakutana na changamoto njiani hasa wa kike na hivyo kusababisha wengine kukatisha masomo ila sasa hivi mambo yamerahisishwa”. alisema Getruda Masawe
Naye mwanafunzi wa shule ya sekondari Mkawaya ameleza kuwa shule hiyo imekuwa msaada kwao kwasababu imerahisisha kufika shuleni kwa wakati na kusoma kwa utulivu bila kuwa na msongamano madarasani.
“shule hii mpya imepunguza uchelewaji wa baadhi ya vipindi hasa vya asubuhi na kwasasa tunahudhuria vipindi vyote bila kuwa na changamoto yoyote amesema Jackline Joseph
Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 inasisitiza mwanafunzi kuwekewa mazingira yanayo mwezesha kupata elimu na mafunzo na kumaliza mzunguko wa elimu katika ngazi husika.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai