Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, imepokea chanjo maalum kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa wa mapafu kwa ng’ombe, ujulikanao kitaalamu kama CBPP, ambapo ng’ombe elfu 88 wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja na chanjo hiyo.
Kwa mujibu wa Kaimu Afisa Mifugo wa Wilaya hiyo, Bi. Magreth Ludovick, chanjo hiyo inalenga kuimarisha afya ya mifugo na kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama kwa wafugaji wa Wilaya ya Hai.
> “Tunashukuru Wizara ya Mifugo kwa kutupatia chanjo hizi muhimu. Itasaidia kudhibiti ugonjwa wa CBPP ambao umekuwa changamoto kwa wafugaji. Tunawahimiza wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi hili na kufuga kwa kufuata ushauri wa kitaalam,” amesema Bi. Ludovick.
Chanjo hizo zimefikishwa wilayani Hai kupitia kampuni ya Hester Biosciences Africa Ltd, ambapo mwakilishi wa kampuni hiyo, Bwana Ahadhi Mwakalobo, amethibitisha kuwa wamekabidhi chanjo aina ya CBPP Vial 880 yenye jumla ya dozi 88,000, ambazo zinalenga kuchanja ng’ombe elfu 88.
> “Chanjo hii ni mahsusi kwa kundi hili la ng’ombe, na ni hatua muhimu katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa mapafu kwa ng’ombe,” amesema Bwana Mwakalobo.
Zoezi la utoaji wa chanjo litaanza mara moja chini ya usimamizi wa maafisa mifugo wa kata na vijiji, huku wafugaji wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kuhakikisha mifugo yao inapata chanjo kwa wakati.
Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha afya ya mifugo na kuinua uchumi wa wafugaji katika Wilaya ya Hai.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai