Mkuu wa Wilaya ya Hai, Haasan Bomboko, amewataka vijana waliojiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba kuwa mfano wa uzalendo, uaminifu, na nidhamu ndani ya jamii wanazotoka, huku akisisitiza kuwa mafunzo hayo ni hatua ya awali ya kuandaliwa kwa ajili ya kulitumikia taifa.
Akizungumza katika kijiji cha Kware leo wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya Jeshi la Akiba kwa vijana, DC Bomboko alisema kuwa nafasi hiyo si ya kawaida, bali ni mwito wa kuitumikia nchi kwa uadilifu na moyo wa kujitoa.
> “Lazima kila mmoja ajue kuwa mko hapa kama sehemu ya awali ya kujifunza uzalendo kwa nchi yenu. Nendeni mka itumikie nchi yenu, mka ilinde nchi yenu na rasilimali zake,” alisema Bomboko.
Aliongeza kuwa askari wa Jeshi la Akiba anatakiwa awe mtu anayeaminika na kukubalika na jamii, na kamwe hawezi kupata heshima hiyo bila kuwa muadilifu.
> “Huwezi kuaminika kwenye jamii yako kama si muadilifu. Imani ya mtu hupatikana kwa kuitafuta kwa vitendo na mwenendo wako mzuri,” alisisitiza.
Katika maelezo yake, Bomboko aliweka wazi kuwa sifa ya kwanza kwa mwanajeshi ni nidhamu, na kwamba mtu asiye na nidhamu hawezi kuwa askari. Alionya dhidi ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu au kuwalinda wahalifu, akisema hilo linakiuka misingi ya maadili ya kijeshi.
> “Sio askari wa Jeshi la Akiba unamwona mtu ni mhalifu halafu unamlinda, au wewe mwenyewe unakuwa sehemu ya uhalifu. Nidhamu hujidhihirisha hata kwa muda – unapaswa kufika mafunzoni saa 11 au 12, si saa moja,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka vijana hao kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
> “Uchaguzi ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania, bila kujali dini, rangi au chama. Hata mtu asiyeamini dini ana haki ya kupiga kura. Vijana mnatakiwa kuwa sehemu ya kutoa elimu hii kwa jamii zenu,” alisema.
Akihitimisha, DC Bomboko aliwataka vijana kutumia kipindi chote cha mafunzo kujijenga kiakili na kiroho ili kuwa raia bora, akisisitiza kuwa maarifa yatakayopatikana yasitumike vibaya, bali yatumike kwa faida ya jamii.
Kitongoji cha Bomani
Anuani ya Posta: 3 RD TTCL RC CHURCH 25382, P.O BOX 27 Hai
Simu: 0754553560
Simu ya Mkononi: 0754553560
Barua Pepe: ded@haidc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Hai